SHIRIKA LA RELI TANZANIA - TRC NA ‘CLOUDS MEDIA GROUP’ (CMG) KUSAFIRISHA MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA KUELEKEA MKOANI KIGOMA



Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na kampuni ya ‘Clouds Media Group’ (CMG) wameandaa treni maalumu itakayobeba mashabiki wa mpira wa miguu kuelekea mkoani Kigoma kutazama mechi kati ya Simba na Yanga itakayochezwa katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani humo siku ya Jumapili Julai 25, 2021.

Treni inatarajiwa kuanza safari katika stesheni ya Dar es Salam kuelekea Kigoma siku ya Ijumaa Julai 23, 2021 na kufika Kigoma siku ya Jumamosi Julai 24, 2021 na baadaye treni hiyo itaanza safari kurudi Dar es Salaam siku hiyo ya Jumapili Julai 25, 2021 majira ya Saa 03:00 Usiku mara baada ya mechi kuisha.

Hivyo, Shirika linawakaribisha mashabiki wa mpira wa miguu na wananchi wote kusafiri na treni ya Deluxe kuelekea Kigoma ambapo tiketi zitapatikana katika stesheni za Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora na Kigoma. Pia wananchi wanaweza kukata tiketi kwa njia ya mtandao kwa kubofya kiungo hiki booking.trc.co.tz.

Gharama za usafiri kwenda na kurudi ni kama ifuatavyo, Daraja la Tatu kwa TZS. 100,000/=, Daraja la Pili Kukaa kwa TZS. 120,000/= na Daraja la Pili Kulala kwa TZS. 150,000/=, pia tiketi za kiingilio katika mechi zitauzwa ndani ya treni.

Treni hiyo itakuwa na burudani kadhaa ikiwemo muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali, mchezo wa bao, drafti, karata, chakula pamoja na vinywaji mbalimbali, TRC inawakaribisha wadau wa Shirika kufadhili na kushiriki katika safari hiyo ya kihistoria.

TRC na CMG wameandaa utaratibu wa kuwawezesha wadau watakaofadhili safari hiyo kujitangaza kupitia ‘Clouds Media Group’ (TV, Radio na Digital Media) na kurasa za mitandao ya kijamii ya TRC (Facebook, Instagram, Twiter, Linkedin na TRC Reli TV - YouTube) pamoja na nafasi ya kuweka mabango ya matangazo katika stesheni za Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora na Kigoma.

Post a Comment

0 Comments