Mfadhili wa zamani wa Simba Azzim Dewji amesema hakufurahishwa na kitendo kilichofanywa na winga wa timu hiyo Bernard Morrison alipoamua kuvua kaptula yake.
Morrison mara baada ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga na kuchukua ubingwa wa (ASFC) juzi aliamua kuvua kaptula yake na kubaki na jezi ya juu na nguo ya ndani huku akishangilia ushindi huo.
Akizungumzia tukio hilo Dewji amesema Morrison hakupaswa kufanya hivyo kwani hatua hiyo ilikuwa ni sawa na kuivunjia heshima klabu yake.
Dewji amesema winga huyo anapaswa kubadilika katika tabia yake kwani matukio ya namna hiyo yanaweza kupoteza thamani yake kwa baadhi ya watu wanaopenda kuona jamii inakuwa na heshima.
Kiongozi huyo amesema hana shida na ubora wa Morrison uwanjani na kwamba matukio ya namna hiyo yanaweza kuwa shuida hata kwa klabu yake kwa watu wengine wanaoiheshimu Simba.
"Sikuunga mkono kitendo kile hakikuwa kitu kizuri kwa uso wa watu walioona kile alichofanya,Simba sasa ni klabu kubwa matukio ya namna ile mtu mwingine anaweza kuuliza yule mchezaji wa Simba?Baada ya hapo anaweza kuidharau klabu,"amesema Dewji.
"Morrison ni mchezaji mzuri na mkubwa anatakiwa kuwa mfano mzuri kwa wengine kwa utamaduni wetu kile sio kitu sahihi na nadhani anatakiwa kubadilika haraka."
0 Comments