Kauli ya Kocha Gomes Kuelekea Mechi ya Fainali FA dhidi ya Yanga




Kuelekea mchezo wa Fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Yanga utakaopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Kocha Mkuu, Didier Gomes ameweka wazi kuwa kikosi chake kitaingia kivingine ili kuhakikisha kinatwaa ubingwa.


Gomes amesema anawaamini wachezaji wake sababu wana uwezo mkubwa na morali ya hali ya juu huku kila mmoja akitaka ubingwa.


Gomes ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini ili kuonyesha wao ni timu bora msimu huu wanapaswa kushinda na kutimiza malengo waliyojiwekea.


“Tunataka kumaliza msimu huu vizuri, tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu lakini pia ni muhimu sana kushinda kombe hili ili iwe mara ya pili mfululizo.


“Kesho (Leo) tutakuwa na mchezo wa aina nyingine na nawaamini wachezaji wangu wanataka kushinda,” amesema Kocha Gomes.


Kwa upande wake Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema maandalizi waliyopata ni mazuri na wapo tayari kutimiza jukumu lililopo mbele yao.


“Maandalizi yameenda vizuri na sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri. Tunajukumu kubwa kwa timu yetu na kufanya vizuri kesho (Leo) ndiyo italeta taswira ya ukubwa wa Simba,” amesema Zimbwe Jr

Post a Comment

0 Comments