Nabi na Mugalu Watwaa Tuzo Ligi Kuu Tanzania Bara.



MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba SC ya Dar es Salaam, Mutshimba Mugalu amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Julai wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), msimu wa 2020/21, huku Mohamed Nasreddine Nabi wa Yanga akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Mugalu alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake mwezi Julai na kuonesha kiwango cha kuvutia akifunga mabao matano, ambapo Simba ilicheza michezo mitano ikishinda mitatu, sare moja na kupoteza mmoja. Wengine walioingia fainali ni Charles Ilamfya wa KMC na Juma Liuzio wa Mbeya City.

Kwa mwezi Julai Simba ilizifunga Coastal Union 2-0, Namungo 4-O na KMC 0-2, kisha kutoka 1-1 na Azam na kufungwa 0-1 na Young Africans SC.

Kwa upande wa Nabi aliiogoza Yanga kushinda michezo mwili na kutoka sare mmoja ikiifunga Simba mabao 0-1, Ihefu mabao 2-0 na kutoka 0-0 na Dodoma Jiji. Aliwashinda Didier Gomes wa Simba na Mathias Lulle wa Mbeya City.

Wachezaji ambao wametwaa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni Prince Dube (Septemba), Mukoko Tonombe wa Yanga (Oktoba), John Bocco wa Simba (Novemba), Saido Ntibazonkiza wa Yanga (Disemba), Deogratius Mafie wa Biashara (Januari), Anuary Jabir wa Dodoma Jiji (Februari), Luis Miquissone wa Simba (Machi), Clatous Chama wa Simba (Aprili), Prince Dube wa Azam (Mei) na John Bocco wa Simba (Juni).

Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedric Kaze aliyekuwa Yanga (Oktoba), Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting (Novemba), Cedrick Kaze aliyekuwa Yanga (Disemba), Francis Baraza aliyekuwa Biashara (Januari), Zuberi Katwila wa Ihefu (Februari), Mohammed Badru aliyekuwa Gwambina (Machi), Didier Gomes wa Simba (Aprili), George Lwandamina wa Azam (Mei) na Didier Gomes wa Simba (Juni).

Wakati huohuo, Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Modestus Mwaluka, kuwa mshindi wa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Julai. Ushindi wa Meneja huyo umefuatia kufanya kwake vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo iliyofanyika kwenye uwanja huo kwa Juni pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Post a Comment

0 Comments