UFADHILI WA MASOMO KWA WATENDAJI KATA 2021-2022



MPANGO WA UDHAMINI WA MASOMO KWA WATENDAJI WA KATA KWA MWAKA
WA MASOMO 2021/2022

1. Kuhusu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) ni chuo cha umma ambacho hutoa mafunzo ya elimu ya juu kwa njia ya Huria na masafa. Chuo kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 17 ya mwaka 1992. Sheria hii ilibadilishwa na Hati Idhini ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ya Januari 2007 ambayo iko sambamba na Sheria ya Vyuo Vikuu Namba 7 ya mwaka 2005. Chuo kina sera mbalimbali na miongozo ya kiutendaji ambayo huongoza utendaji wake ili kuimarisha ubora wa utoaji wa elimu na majibu ya haraka kwa wateja wake na jamii kwa ujumla. Chuo kina ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina vituo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na vituo vya Uratibu Unguja, Pemba, Kahama na Tunduru. 

Dira ya CKHT, “kuwa chuo kikuu kinachoongoza katika utoaji wa elimu kwa njia ya mtandao katika kukuza na kutumia Maarifa” imekifanya chuo kiwe cha kipekee Tanzania na hata Afrika Mashariki. Chuo kina nafasi ya kipekee kama taasisi ya elimu ya juu kuwa mstari wa mbele kuiweka Tanzania katika nchi ya uchumi wa kati unaochagizwa na viwanda kwa kutoa wahitimu wenye jukumu kubwa la kuifanya nchi iweze kufanikisha dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. CKHT kipo mstari wa mbele katika kukuza maarifa na kupanua wigo wa upatikanaji wa Elimu ya Juu kwa wananchi wa Tanzania ambayo pia ni azma ya viongozi wa nchi wa sasa na wa baadaye. CKHT kinatumia mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji inayoweza kuwafikia wananchi wengi kule kule walipo wakiendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa huku wakijiendeleza kielimu.

2. Mpango wa Udhamini wa Masomo kwa Watendaji wa Kata

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kinalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza fursa na upatikanaji wa elimu ya juu yenye ubora na nafuu kupitia mpango wa udhamini wa masomo kwa watendaji wa kata na masheha. Lengo la udhamini ni kuimarisha uwezo wa rasilimali watu kwa kupata maarifa na ujuzi stahiki ili kukuza uchumi wa viwanda katika nchi. Walengwa wakuu katika mpango huu ni watendaji wa kata (Tanzania Bara) na shehia (Zanzibar) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpango huu ulianza mwaka wa masomo 2020/2021.

Muundo wa mpango huu kwa watakao kidhi vigezo vya udhamini na udahili ni punguzo la asilimia 100 ya ada kwa watendaji kata na masheha katika programme yoyote ya astashahada, stashahada, shahada ya kwanza au shahada za Uzamili na Uzamivu zinazotolewa na CKHT. Udhamini utatolewa kwa Watendaji wa kata watano (5) au Masheha watano (5) kwa kila halmashauri ya mji au wilaya.

2.1 Vigezo Stahiki kwa Watendaji na Masheha

i) Muombaji lazima awe Mtendaji wa kata au Shehia
ii) Muombaji lazima awe na ushahidi wa ushiriki wake katika kukisaidia CKHT katika juhudi zake za kuhamasisha na kuelimisha jamii kujiunga na elimu ya mtandao, huria na masafa kwa kusaidia angalau udahili wa wanafunzi kumi (10) kutoka eneo lake.
iii) Mtendaji wa kata au Sheha lazima athibitishwe na apewe kibali na mwajiri wake kutoka wilaya au manispaa husika kulingana na kanuni na taratibu na kazi kabla ya kuomba udhamini. Muombaji lazima akidhi vigezo vya udahili katika kada ya masomo atakayochagua kama ilivyoainishwa katika Prospectus ya CKHT.
iv) Waombaji watakaofanikiwa watapata punguzo la ada kwa asilimia mia moja (100%) kwa mwaka lakini watatakiwa kulipa tozo zingine za mitihani, serikali ya wanafunzi, kitambulisho, mahafali, na ada ya hati ya matokeo.
v) Muombaji lazima awe na uwezo wa kumaliza masomo katika muda uliopangwa.

3. Taratibu za Kutuma Maombi

i) Hakuna gharama ya maombi.
ii) Waombaji lazima watume barua za maombi kwa waajiri wao ili kuhakikiwa na kuthibitishwa kwa ajili ya kuomba udhamini wa masomo.
iii) Watakaofanikiwa kuteuliwa na wilaya au mamlaka zao watatakiwa kujaza na kutuma fomu ya maombi ya udahili na udhamini ambazo zinapatikana kwenye vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania vilivyoko katika mikoa yote Tanzania bara na vituo vya uratibu vya Unguja, Pemba, Kahama na Tunduru.

4. Muda wa maombi ya udhamini kwa mwaka wa masomo 2021/2022

i) Wanaoingia Oktoba : Tarehe ya mwisho wa maombi ni 20/09/2021
ii) Wanaoingia Aprili: Tarehe ya mwisho wa maombi ni 27/02/2022

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na;
Mkurugenzi wa Masomo ya Astashahada, Stashahada na Shahada za Awali,
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,
Kinondoni Biafra, Barabara ya Kawawa,
S.L.P 23409, DAR ES SALAAM, TANZANIA.

Post a Comment

0 Comments