Wachezaji Simba wapewa Mapumziko Siku 10

 


MENEJA wa Klabu ya Simba SC, Patrick Rweyemamu amesema kuwa wachezaji wa Klabu hiyo wamepewa mapumziko ya siku 10 baada ya kukamilisha msimu kwa kutwaa mataji yote mawili, Ligi Kuu na Kombe la FA.

“Baada ya siku 10 tutaanza kujikusanya kuanza maandalizi ya msimu ujao (2021/2022). Unajua sisi tuna malengo makubwa siku zote, tunajua michuano ya ligi ya mabingwa itaanza mapema hivyo tutapaswa kurejea mapema kujiandaa,” amesema Rweyemamu.

Akizungumzia ubingwa wa FA walioupata mbele ya Yanga, Rweyemamu amesema ni jambo la kujivunia kwa Simba kushinda ubingwa huo mbele ya watani zao na kikubwa zaidi ni kuwa wameweza kuwabeba Yanga kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao.

“Mechi hizi za derby huwa hazizoeleweki, lazima tuwaheshimu Yanga kwa sababu ni timu kongwe kama tulivyo sisi hivyo hatukutarajia mchezo mwepesi. Lakini jambo kubwa kwetu tuliweza kupata ushindi dhidi yao na kufanikiwa kutetea taji la FA”

“Lakini pia tunaweza kusema tumewabeba kwenda kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao. Hawa ni watani zetu pengine wangeshinda wangeweza kusema wametumia nguvu zao lakini hilo halipo tena, itabaki kwenye historia kuwa tumewabeba kushiriki michuano ya CAF,” alitamba Rweyemamu

Michuano ya ligi ya mabingwa itaanza mwanzoni mwa mwezi September kwa mechi za hatua ya awali kupigwa. Simba ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki kuanzia hatua ya awali.

Ni timu tatu tu ambazo hazitashiriki hatua hiyo msimu ujao ambao ni Al Ahly (mabingwa CAF CL), Esperance na Wydad Athletics.

Post a Comment

0 Comments