Mgunda awapa mikakati Coastal Union



BAADA ya kufanikiwa kuibakisha Ligi Kuu, Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda, ameutaka uongozi wa timu hiyo kuweka mikakati kabambe ya kuhakikisha wanafanya usajili wa nguvu ili hali hiyo isijirudie tena siku zijazo.


Coastal Union ililazimika kucheza mechi za mtoano ( Play Off) dhidi ya timu ya Pamba FC ya Mwanza ili kubaki Ligi Kuuu, baada ya kumaliza ligi ya msimu uliopita ikiwa ya 14.


Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Mgunda amesema kilichochangia timu hiyo kuangukia kwenye hatua hiyo ni kukosa wachezaji wenye uzoefu, jambo ambalo limemsumbua karibu msimu mzima.


“Niwapongeze wachezaji kwa kujitoa kuipigania timu kwa kipindi chote ikiwemo mechi hizi mbili za mtoano, lakini uongozi lazima ukutane na kuweka mikakati ya kuijenga timu ili msimu ujao hali hii isijekujirudia,” alisema Mgunda.


Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na Ligi Kuu Tanzania Bara, alisema kitu cha msingi ambacho kinatakiwa kufanywa ni kuhakikisha wanafanya usajili wa wachezaji hata sita wenye uzoefu na kuongezea na vijana waliopo, anaamini timu hiyo itafanya vizuri kama ilivyokua misimu miwili iliyopita.


Mgunda alisema kucheza ni sawa na pata potea na timu yoyote inaweza kushinda na kujikuta wanashuka daraja, hivyo itakuwa vyema uongozi wa timu hiyo na wadau wake kuongeza bidii za kuipambania timu yao ili hali hiyo isijirudie msimu ujao.


Katika mechi za mtoano dhidi ya Pamba, Coastal Union ilifuzu kwa matokeo ya jumla ya mabao 5-3, mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Nyamagana timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na katika mchezo wa marudiano uliopigwa Dimba la Mkwakwani Tanga, Coastal iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Post a Comment

0 Comments