Simba mabingwa Kombe la FA




TIMU ya Simba imefanikiwa kutetea taji lake la ubingwa wa Kombe la FA , baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Ushindi huo umeifanya Simba kuzima shangwe na kejeli za mashabiki wa Yanga, ambao kabla ya mchezo huo, wiki mbili zilizopita iliwafunga watani zao hao kwa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni.

Hilo ni taji la tatu kwa Simba msimu huu baada ya kuanza na Ngao ya Jamii kwa kuifunga Namungo FC, kisha ikafanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu wiki iliyopita kabla ya jana kufunga na Kombe la FA.

Hayo ni mafanikio makubwa kwa Kocha Didier Gomes wa Simba, ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni na kutwaa mataji mawili ya timu hiyo, ikiwemo kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kiungo Taddeo Lwanga ndiye aliyepeleka huzuni Jangwani kufuatia bao alilofunga kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Lius Miquissone, dakika ya 79 na mpira kumpita kipa wa Yanga, Faruk Shikalo.

Yanga ambayo katika mchezo huo ilicheza pungufu kwa dakika 47, baada ya kiungo wake mkabaji, Mukoko Tonombe kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko nahodha wa Simba, John Bocco dakika ya 43, ilionekana kucheza vizuri katika kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi kadhaa lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia ipasavyo.

Katika kipindi hicho cha kwanza, timu zote zilioonekana kupaniana na kusababisha rafu nyingi kwa kila upande jambo ambalo lilipoteza ladha ya mchezo.

Mshambuliaji wa Simba, Chris Mugalu alipata nafasi kadha kipindi cha kwanza, lakini alishindwa kuzitumia ipasavyo, huku Luis Miquissone naye akikaribia kuisababishia timu yake mkwaju wa penalti baada ya kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari na Bakari Mwamnyeto, lakini mwamuzi Ahmed Arajiga alikataa.

Baada ya milango ya timu zote kuwa migumu dakika ya 65 ya kipindi cha pili kocha wa Simba alifanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Larry Bwalya na kumuingiza Bernard Morisson, ambaye kwa kiasi fulani alionekana kuichachafya ngome ya Yanga lakini alikutana na ukuta mgumu wa Yanga.

Simba ilionekana kurudi kwa kasi kipindi cha pili baada ya kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Yanga ambayo ilionekana kucheza kwa kujihami huku wakitegemea mashambulizi ya kustukiza, ambayo hata hivyo hayakuwa na madhara kwenye lango la Simba.

Mshambuliaji Yacouba Sogne aliweza kupata nafasi nzuri ya kuifungia timu yake bao dakika ya 64, lakini shuti alilopiga lilipaa kidogo juu ya lango la Simba, ambalo lilikuwa likilindwa na kipa Aisha Manula ambaye muda mwingi wa kipindi cha pili alikuwa mapumzikoni.

Mchezaji Tadeo Lwanga aliibuka mchezaji bora na kuzawadiwa 1,000,000 na banki ya KCB.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kuifunga Yanga katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam mfululizo, kwani mwaka jana waliondoshwa katika hatua ya nusu fainali kwa mabao 4-1.

Simba pamoja na kutwaa ubingwa huo, lakini hawatashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa pamoja na Yanga huku Azam na Biashara zikiangukia katika Kombe la Shirikisho

Post a Comment

0 Comments