USAJILI wa Yanga sasa ni kama viongozi wameamua kufanya kimafia kwani kesho Ijumaa wanatarajiwa kusafiri kwenda nchi za Afrika Kusini, Morocco na Congo Kinshasa kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili za wachezaji wao.
Yanga tayari imemalizana na wachezaji wa kigeni Shaban Djuma Fiston Mayele na Francis Kazadi wote kutoka Congo na Anthony Akumu wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Wachezaji wazawa waliomalizana na Yanga ni beki wa KMC, David Bryson na kiungo mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mshauri wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema kuwa leo wanatarajiwa kukutana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kwa ajili ya kupitia ripoti yake ya usajili kabla ya keshokutwa Ijumaa kukamilisha.
Senzo alisema kuwa Ijumaa yeye huenda akarejea nyumbani kwao Afrika Kusini kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji Akumu atakayekuja kuichezea Yanga.
Aliongeza kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa timu hiyo, Injinia Hersi Said yeye atakwenda Morocco na Kaimu Katibu Mkuu, Haji Mfikirwa ambaye atakwenda Congo kukamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji waliofikia makubaliano mazuri.
“Kama uongozi tumeandaa utaratibu mpya wa usajili, hivyo kesho (leo) tutakutana na kocha kwa ajili ya kuipitia ripoti yake.”
Aidha Championi lilizungumza na Mayele kuhusu mipango yake namna ya kuwakabili walinzi wa Simba ambapo alisema: “Nimekitazama kikosi cha Yanga, nina uhakika wa kupata nafasi ya kucheza nikiwa kama mshambuliaji, nipo tayari kukabiliana na changamoto za ligi kuu hivyo sijali kukutana na mabeki wa timu yoyote ikiwemo Simba kwani nipo tayari kwa mapambano.”
0 Comments