Manara Out Simba Sc



Klabu ya Simba imemteua Ndugu Ezekiel Kamwaga kuwa Kaimu Mkuu wa ldara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu kwa kipindi cha miezi miwili. Katika kipindi hicho, Kamwaga atashiriki katika maboresho ya muundo na utendaji wa Idara hiyo. 

Kamwaga ni mwandishi wa habari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 kwenye tasnia ya habari - akifanya kazi katika vyombo vya habari vya ndani na kimataifa. Kamwaga anaijua vizuri Klabu ya Simba na historia yake kwani amewahi kuitumikia katika nafasi za Msemaji wa Klabu na Kaimu Katibu Mkuu wa Simba.

Wakati huo huo, Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, kwa kauli moja, imeridhia matakwa ya Ndugu Haji Manara ya kutoendelea kuhudumu katika nafasi ya Msemaji wa Klabu. Bodi inamshukuru kwa maneno aliyoyatumia kuwaaga wana-Simba katika kundi la viongozi wa Simba (Simba HQ) na kwa kazi aliyoifanyia Klabu katika kipindi alichoshika nafasi hiyo, na inamtakia heri katika shughuli zake.

Mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya ldara ya Habari na Mawasiliano na ldara nyingine, Klabu itatangaza fursa mbalimbali za ajira katika kipindi cha wiki chache zijazo.


Imetolewa na:- Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba

28 Julai 2021


Post a Comment

0 Comments